Kwa mujibu wa gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth, Jumuiya ya Magereza ya Kizayuni imepokea amri ya kuwaachilia huru mateka wa Palestina kama vinavyosema vipengee vya makubaliano ya kusimamisha vita yanayojumuisha kuachiliwa huru mateka.
Gazeti hilo limetangaza hayo leo Jumamosi na kuongeza kuwa, mateka wa Palestina wataachiliwa huru kutoka magereza matano ya Israel na tayari mateka hao wameashaanza kutolewa kwenye jela hizo na kupelekea maeneo maalumu ya kuwaachilia huru.
Chombo hicho cha habari cha Kizayuni kimeongeza kuwa: Makubaliano hayo ya kubadilishana mateka yanajumuisha kuachiliwa huru mateka wapatao 250 wa Palestina waliohukumiwa kifungo cha maisha na mateka 1,700 kutoka Ghaza ambao walitekwa na wanajeshi wa Israel baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa ya tarehe 7 Oktoba.
Hapo awali, "Musa Abu Marzouk", mjumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) alikuwa ametangaza kwamba harakati hiyo inashauriana na wapatanishi ili kuondoa vikwazo na kuandaa njia ya kuachiliwa huru viongozi mashuhuri wa Palestina ambao wako katika jela za kuogofya za Israel.
Ameongeza kuwa: Marwan Barghouti, Ahmed Saadat na Abbas al-Sayyid ni miongoni mwa viongozi mashuhuri wa Palestina ambao utawala wa Kizayuni unakataa kuwaachilia huru.
Your Comment